Mkurugenzi
Mtendaji wa Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS), Eng. Patrick Mfugale
akitoa maelezo kwa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli, wakati wa hafla ya
uwekaji wa jiwe la Msingi ujwenzi wa Barabara ya Juu (FlyOver) kwenye
makutano ya Barabara ya Mandela na Nyerere, eneo la Tazara, Jijini Dar
es salaam leo.
****
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Magufuli ameweka jiwe la
msingi kwa ajili ya kuanza rasmi ujenzi wa barabara ya juu kwenye
makutano ya barabara za Nyerere na Mandela eneo la Tazara jijini Dar es
Salaam leo.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Rais Magufuli
amesema ujenzi huo wa barabara ya juu utaanza mara moja kwa ushirikiano
na serikali ya Japan na utagharimu Shilingi 100 bilioni.
Amesema, serikali ya Japan imefadhili mradi huo kwa Sh 93.44 bilioni wakati serikali ya Tanzania imechangia Sh 8.36 bilioni.
Rais
amewataka wananchi watakaopata ajira kwenye ujenzi wa mradi huo wawe
waaminifu na wasiwe wezi wa mafuta, vifaa vya ujenzi au kuendekeza
migomo.
“Pia serikali ya awamu ya tano imetenga Sh 1 trilioni
kuanza ujenzi wa reli ya kisasa (standard gauge) kwa reli ya kati.
Tutajenga kituo kikubwa Ruvu ili mizigo isafirishwe kwa njia ya reli
kutoka bandari ya Dar es Salaam hadi Ruvu na malori yatakuwa yakichukua
mizigo pale, jambo hili litasaidia kupunguza foleni hapa Dar es Salaam,” alisema Rais Magufuli.
Aidha
ameishukuru serikali ya Japan kwa ufadhili wa miradi ya maendeleo
nchini kwa zaidi ya miaka 36. Amesema Japan imekuwa ikiisaidia Tanzania
bila masharti kama ilivyo kwa baadhi ya wafadhili wa maendeleo.
Akionyesha kukerwa na wafadhili wanaotoa misaada yenye masharti na vitisho, Rais Magufuli amesema; “Ni bora kula muhogo wa kujitafutia kuliko kula mkate kwa masimango.”
(source mpekuzi)
No comments:
Post a Comment